mtwara regional referral hospital
(ligula RRH)

ujue ugonjwa wa Ebola

Utangulizi

Ebola ni ugonjwa hatari unaosababishwa na virusi vujulikanavyo kitaalam kama (Ebola Virus). Ugonjwa huu ni miongoni mwa magonjwa yajulikanayo kwa ujumla kama Homa za virusi zinazosababisha kutoka damu sehemu za wazi za mwili mfano puani , masikioni , na machoni. Ugonjwa huu unaathiri binadamu na wanyawa kama vile nyani , ngedere , sokwe na popo.


Mlipuko mkubwa kuwahi kuokea duniani umeokea katika nchi za Liberia , Sierra Leone na Guinea.

Mlipuko huu pia umeaziathiri nchi za Nigeria , Senegal , Mali na Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo , pia nje ya bara la Afrika nchi za Marekani na Uispania zimeathirika.

Ugonjwa wa Ebola umetoka katika nchi jirani za Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo . Kutokana na muingiliano kati ya nchi na nchi , kuna uwezekano mkubwa wa ugonjwa huu ukaenenea nchi nyingine endapo tahadhari hazitachukuliwa.


Jinsi Ebola inavyoambukizwa

Ugonjwa wa Ebola unaambukizwa kwa haraka kutoka mtu mmoja aliye na virusi vya Ebola hadi mwingine kupitia njia zifuatazo:-

  • Kugusa majimaji ya mwili toka kwa mtu aliyeambukizwa virusi vya Ebola –mfano damu , matapishi ,       jasho , mkojo , mate , machozi na kamasi.
  • Kugusa au kuosha maiti ya mtu aliyefariki kwa ugonjwa wa Ebola
  • Kugusa godoro, shuka , blanketi au nguo zilizotumiwa na mgonjwa wa Ebola
  • Kuchomwa  na sindano au vifaa visivyo safi na salama ambayo vimetumiwa na mgonjwa  wa Ebola
  • Kugusa mizoga au kula wanyama pori kama vile sokwe , Nyani  na Popo
  • Kula matunda yaliyoliwa nusu na wanyama


Dalili za Ebola

Dalili za ugonjwa wa Ebola huanza kujitokeza kati ya siku 2 hadi 21 baada ya kupata maambukizi. Mgonjwa wa Ebola huwa na dalili zifuatazo

  • Homa kali ya ghafla
  • Maumivu ya kichwa
  • Maumivu ya mwili , misuli na viungo
  • Kuharisha (kunakoweza kuambatana na damu)
  • Kutapika (kunakoweza kuambatana na damu)
  • Vipele mwilini
  • Kuvia damu chini ya ngozi au kutokwa na damu puani , mdomoni , machoni na masikioni.

TIBA

Ugonjwa wa Ebola hauna tiba maalum wala chanjo , Mgonjwa hupatiwa tiba saidizi kulingana na dalili alizonazo , kama vile

  • Tiba ya kushusha homa na maumivu
  • Kuongezewa damu na maji mwilini
  • Tiba lishe

Kujikinga na Ebola

  • Epuka kusalimiana kwa kushikana mikono au kukumbatiana
  • Epuka kugusa damu , matapishi , mkojo ,kinyesi , kamasi , mate , machozi na maji mengine yanayotoka mwilini mwa mtu mwenye dalili za ugonjwa huu.
  • Epuka kugusa au kuosha maiti ya mtu aliyekufa akiwa na dalili za Ebola badala yake toa taarifa kwa uongozi wa serikali ili wasimamie taratibu za mazishi
  • Epuka kutumia nguo , shuka , blanketi , kitanda na godoro za mtu aliyeambukizwa ugonjwa huu.
  • Nawa mikono kwa maji yanayotiririka na sabuni mara unapomembelea mgonjwa hospitalini au kumdumia nyumbani
  • Epuka kugusa wanyama kama vile popo , nyani , sokwe ,tumbili na swala au mizoa ya wanyama
  • Zingatia ushauri na maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya na viongozi wa serikali kuhusu ugonjwa wa Ebola
  • Wahi kituo cha kutolea huduma za afya uonapo dalili za ugonjwa wa Ebola
  • Toa taarifa mapema kwenye kituo cha huduma za afya, ofisi ya serikali ya mtaa au kijiji uonapo mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola au kifo.
  • Zingatia usafi binafsi pamoja na usafi wa mazingira yako


Athari za Ebola

  • Ebola husababisha unyanyapaa kwa waathirika na familia zao
  • Ebola husababisha athari za kisaikolojia kwa waathirika , familia zao , na jamii
  • Huenea kwa haraka sana na kusababisha vifo vingi na kuathiri nguvu-kazi ya taifa
  • Jamii huingiwa na hofu na wasiwasi na kushindwa kufanya shughuli za kiuchumi na kujiingizia kipato
  • Ni gharama kubwa kuhudumia wagonjwa wa Ebola


Wajibu wa jamii

  • Nenda haraka kwenye kituo cha kutolea huduma za afya  pindi unapohisi kuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola, au unapogusana na mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola.
  • Toa taarifa mapema kwenye kituo cha huduma za afya ,ofisi ya serikali ya mtaa au kijiji uonapo mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Ebola au kifo.
  • Epuka uvumi , tafuta taarifa sahihi kuhusu ugonjwa wa Ebola toka kwa mamlaka husika.